tangazo

Thursday, 12 December 2013

AJALI YA BASI TANGA YAUA 12 NA KUJERUHI 44

    Basi lilopata ajali likiwa limeharibika vibaya

 Watu 12 wamekufa na wengine 44 wamejeruhiwa vibaya baada ya basi la kampuni ya Burdan linalofanya safari zake kutoka wilayani Korogwe kwenda jijini Dar es salam kuacha njia kisha kupinduka.

Ajali hiyo imetokea eneo la kijiji cha Taula kilichopo kata ya Kwedizinga wilayani Handeni katika barabara kuu inayounganisha Chalinze-Segera ambapo inadaiwa kuwa dereva wa basi hilo ambaye ni miongoni mwa marehemu alikwaruzwa na lori wakati alipokuwa akilipita lori kubwa aina ya Fuso ndipo gari lilipomshinda na kusababisha kwenda katika bonde lililopo pembeni mwa barabara hiyo.

Baadhi ya watu waliokua majeruhi katika eneno la tukio wamesema waliokufa pale pale baada ya gari kupinduka walikuwa sita lakini wengine waanne walikuwa katika hali mbaya ndipo wakati wakiwa katika harakati za kuwawahisha hospitali walipoteza maisha.

 Madaktari wakimhudumia mmoja kati majeruhi 

Kwa upande wa daktari wa zamu aliyepokea miili ya marehemu na majeruhi katika hospitali teule ya wilaya ya Korogwe ya Magunga Dr, John Hedes hakusita kuwataja waliofariki dunia kwa majina ambapo ni wanaume sita na wanawake sita huku wengine sita wamejeruhiwa vibaya na kuhamishiwa katika hospitali za rufaa za KCMC na Muhimbili.

Kufuatia hatua hiyo,kamanda wa polisi mkoani Tanga Costantine Massawe amewataka abiria wanaosafiri katika mabasi ya kampuni mbali mbali mkoani Tanga kupiga namba za simu za askari yeyote alieyeko katika eneno lao ili dereva anayekwenda mwendo kasi aweze kukamatwa.

Tayari rais Jakaya Kikwete amemtumia mkuu wa mkoa wa Tanga salam za rambirambi kufuatia ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu 12 na kujeruhi wengine 44.


  Wananchi wakiwa nje ya hospitali korogwe

No comments: